Wilaya ya Kondoa Mkoani Dodoma imeitikia agizo la Mhe. Rais Magufuli la kumaliza tatizo la njaa kwa kuzindua mkakati wa kilimo na usalama wa chakula kwa mwaka 2016.
Kikao cha Baraza la Madiwani wa Wilaya hiyo kilichofanyika mwishoni mwa wiki kwa kauli moja kilipitisha/kiliidhinisha mpango mkakati huo wa kilimo na usalama wa chakula ulioandaliwa na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa.
Taarifa ya Halmashauri ya Wilaya Kondoa inabainisha kuwa Mkakati huo utaanza kutumika msimu huu wa kilimo wa 2015/2016 ambapo inaaaminika unaweza kutokomeza tatizo la upungufu wa chakula kwa kuwa Kondoa ina maeneo ya kutosha yanayofaa kwa kilimo na yenye hali ya hewa nzuri ukilinganisha na maeneo mengine ya Mkoa wa Dodoma.
Mpango Mkakati huo wa Kilimo na Usalama wa Chakula unalenga kila msimu wa kilimo, kila kaya pamoja na mazao mengine, inatakiwa kulima na kupanda ekari moja ya mojawapo ya mazao ya Mtama, Uwele, Muhogo na Viazi vitamu ambapo tayari Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa imezindua shamba darasa la mbegu bora ya Mihogo aina ya Mumba kutoka kituo cha utafiti cha Hombolo kwa lengo lakuzalisha mbegu za Muhogo na kuzisambaza Wilaya nzima.
Aidha, Mpango unaelekeza kila kaya kupanda miti ya matunda, kivuli na mbao isiyopungua kumi kuzunguka eneo la makazi au shamba. Vilevile,kila kaya itatakiwa kuweka hifadhi ya chakula kitakachotosheleza kipindi cha miezi ishirini na nne (24) ambapo kiasi cha chini cha hifadhi ni magunia kumi (10) ya kilo mia (100) kila moja.
Wakati wa Mauzo ya Mazao ya chakula ambayo ni ziada, kila kaya ni lazima ipate kibali cha kuruhusiwa kuuza mazao ya chakula kutoka kwa Afisa Mtendaji wa Kijiji au Afisa Ugani wa Kijiji au Kata. Pamoja na mazao, kila kaya inatakiwa kufuga kuku wasiopungua sita.
Baraza hilo la madiwani lilikubaliana kuwa, katika kusimamia utekelezaji wa Mkakati huu, kamati za Maafa za Vijiji na Kata kwa kushirikiana na maafisa ugani, zitafanya ukaguzi wa mashamba ili kubaini wakulima walioitikia na waliokaidi maelekezo. Pia kamati hizi zitafanya ukaguzi wa nyumba kwa nyumba mwezi Oktoba wa kila mwaka kubaini hali ya chakula katika kaya. Taarifa za ukaguzi zitatumwa Wilayani ambapo ukaguzi na tathimini ya hali ya chakula utafanyika.
Kwa mujibu wa Mkakati uliopitishwa na Baraza la Madiwani la Wilaya ya Kondoa, kaya/Mkulima atakaye bainika kutotekeleza mikakati iliyowekwa bila sababu za msingi atapoteza sifa za kusaidiwa  na serikali kupatiwa chakula cha msaada pindi pakitokea upungufu wa chakula.
Pamoja na kupoteza sifa, kaya/mkulima atapewa adhabu ya kufanya kazi ya kijamii kama usafi na ufyatuaji wa matofali kwenye ujenzi wa majengo ya serikali au kulipa faini kwa mujibu wa itakavyoonekana inafaa na baraza la kata.
Mkakati huo pia umeainisha kuwa kila Mtendaji wa Kata, Kijiji na Afisa Ugani atakayeshindwa kusimamia utekelezaji wa mikakati ya kilimo iliyowekwa atachululiwa hatua kali za kisheria kwa mujibu wa sheria za utumishi wa Umma za mwaka 2002 na kanuni za utumishi wa Umma za mwaka 2003. 
 Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Chiku Gallawa, viongozi wa Wilaya ya Kondoa na kijiji cha Mulua Kondoa wakitembelea shamba darasa la mbegu za Muhogo mwishoni mwa wiki Wakati wa uzinduzi wa mkakati wa kilimo na usalama wa chakula Wilayani humo.
 Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Chiku Gallawa, akishiriki zoezi la kupanda mbegu za Muhogo kwa lengo la kuzizalisha kwa wingi kwenye shamba darasa kijijini Mulua Kondoa wakati wa uzinduzi wa mkakati wa kilimo na usalama wa chakula Wilayani humo mwishoni mwa wiki, mbegu hizo zitasambazwa Wilaya nzima.
 Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Shabaan Kissu, akishiriki zoezi la kupanda mbegu za Muhogo kwa lengo la kuzizalisha kwa wingi kwenye shamba darasa kijijini Mulua wakati wa uzinduzi wa mkakati wa kilimo na usalama wa chakula Wilayani humo mwishoni mwa wiki, mbegu hizo zitasambazwa Wilaya nzima.
 Baadhi ya Viongozi wa Wilaya ya Kondoa wakishiriki zoezi la kupanda mbegu za Muhogo kwa lengo la kuzizalisha kwa wingi kwenye shamba darasa kijijini Mulua wakati wa uzinduzi wa mkakati wa kilimo na usalama wa chakula Wilayani humo mwishoni mwa wiki, mbegu hizo zitasambazwa Wilaya nzima.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Chiku Gallawa na viongozi wa Wilaya ya Kondoa, wakishiriki zoezi la palizi kwenye shamba darasa la mahindi kijijini Mulua Kondoa walipotembelea mashamba darasa ya mazao ya chakula wakati wa uzinduzi wa mkakati wa kilimo na usalama wa chakula Wilayani humo mwishoni mwa wiki.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. 'Home sweet home' Nawapongeza sana wananchi wa Wilaya ya Kondoa kwa kuliunga mkono agizo la Mh. Rais wetu la kumaliza tatizo hilo sugu la njaa khususan kwa kuzinduwa mkakati huo wa kilimo na usalama wa chakula kwa mwaka huu 2016. Naamini zoezi hilo litaaimarishwa vilivyo na kuwa endelevu ili kuweza kujikimu na kujihami kwa suala zima la ukame na njaa endapo kutajitokeza dharura zozote zile, mathalan ukosefu wa mvua, wadudu wharibifu wa mazao na mengineyo kadhaa yatukanayo na 'natural disaster'. Kwa kuitikia wito huo wilaya nzima na vitongoji vyake vyote itakuwa imeweza kuwa na uhifadhi mzuri wa akiba ya chakula endapo dharura yeyote itajitokeza.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...