Na Bashir Yakub.
Mara kadhaa kwenye familia mbalimbali kumekuwa hakuna maelewano juu ya nani asimamie mirathi. Unakuta wapo wanaomkubali fulani asimamie na wapo wanomkataa wakimtaka fulani mwingine ndiye asimamie. Hii huwa na athari kubwa sana kwa warithi hasa watoto kama wanasoma ambao kimsingi hutakiwa kutumia mali zile katika mahitaji ya msingi kama ada na mahitaji mengine muhimu ya kiustawi.
Tumeshashuhudia mara nyingi watoto wakiacha kwenda shule kwa kukosa ada na mahitaji mengine muhimu kwa ustawi wao sababu kubwa ikiwa mgogoro wa nani awe msimamizi mirathi. Naamini huwa hakuna sababu za msingi za kufikia huko kwakuwa tayari sheria imetoa mwongozo wa nini kifanyike katika mazingira kama hayo. Utata huu mara nyingi husababishwa na kutokuaminiana hasa kama ndugu wana utofauti wa mmoja wa wazazi mama au baba. Makala yataeleza lipi la kufanya.
1.MAMBO YANAYOZINGATIWA NA MAHAKAMA KUTEUA MSIMAMIZI MIRATHI.
( a ) Kwanza mahakama huangalia kama kuna wosia. Iwapo kuna wosia basi huangalia iwapo wosia ule umemtaja msimamizi wa mirathi. Ikiwa umemtaja msimamizi wa mirathi na hakuna shauri lolote lililofunguliwa kupinga au kuhoji uhalali wa wosia huo basi msimamizi wa mirathi aliyetajwa ndani ya wosia huo ndiye atakayethibitishwa rasmi na mahakama kama msimamizi halali wa mirathi.
( b ) Uadilifu wa mwombaji ni jambo jingine muhimu linalozingatiwa sana na mahakama kabla kumteua msimamizi wa mirathi. Yawezekana mtu akawa ni ndugu wa karibu na wa pekee wa marehemu aliyebaki lakini si mtu muadilifu. Ni mtu ambaye kukabidhiwa amana kubwa ya mirathi ambayo hukusanya magari ,majumba , mashamba viwanja n.k itakuwa ni sawa na kuzitupa mali hizo.
Lakini pia uadilifu asiwe ni mtu ambaye ana upendeleo kiasi akikabidhiwa mirathi hawezi kutenda haki baina ya warithi. Watu wenye sifa hizo hawatateuliwa kusimamia mirathi. Hata hivyo hayo yatatakiwa kuibuliwa na kuoneshwa na wanaompinga msimamizi aliyependekezwa kwa kupeleka pingamizi mahakamani.
( c ) Jingine linaloangaliwa ni maslahi ya muombaji kwa marehemu au kwa mali za marehemu. Maslahi kwa marehemu huangaliwa ukaribu wa udugu kwa mfano huyu ni mjomba wa marehemu na huyu ni mtoto wa marehemu. Kimsingi mtoto wa marehemu atakuwa na nafasi kubwa ya kuwa msimamizi wa mirathi kuliko mjomba wa marehemu. Aidha maslahi kwa mali za marehemu huhusisha wadeni wanaomdai marehemu kwa mfano mabenki n.k. Hawa nao wanaweza kuomba na kukubaliwa kuwa wasimamizi wa mirathi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...