Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii kanda ya kaskazini.

WAKAZI wa kata ya Shirimatunda katika maanispaa ya Moshi, wameingiwa na hofu ya kupoteza maisha yao,kufuatia taarifa za kuwapo kwa mtu anayedhaniwa kuwa na ugonjwa hatari wa Ebola anayehudumiwa katika zahanati ya kata hiyo.


Kutokana na hofu hiyo,halmashauri ya manispaa ya Moshi imelazimika kuifunga kwa muda usiojulikana zahanati hiyo na kuwahamishia wagonjwa katika hospitali nyingine ikiwamo ya St Joseph katika manispaa hiyo.



Ripota wetu ambaye alikuwa eneo la zahanati hiyo alishuhudia baadhi ya madaktari wakiongozwa na mganga mkuu wa manispaa hiyo,Dk Christopher Mtamakaya pamoja na wataalamu wengine wa afya wakifanya kikao cha dharura kujadili hali hiyo.



Kadhalika,waandishi wa habari waliokuwepo katika zahanati hiyo
walishuhudia baadhi ya wataalamu wa afya wakiwa na mavazi rasmi yanayotumiwa na madaktari wanaohudumiwa wagonjwa wa Ebola.



Pamoja na kikao hicho,Zahanati hiyo imewekwa tangazo katika lango kuu linalosomeka 'Huduma zote za afya zimesitishwa kwa muda, Utawala' hali ambayo imeendelea kuzua maswali mengi kwa wagonjwa wanaokwenda kupata matibabu katika zahanati hiyo.



Mwenyekiti wa mtaa wa Kigongoni,kata ya Shirimatunda ilipo zahanati hiyo,Juma Sambeke alisema hajashirikishwa katika maamuzi ya kugeuza Zahanati hiyo kama Karantini ya mtu anayedhaniwa kuwa na Ugonjwa wa Ebola.



Alisema kuwapo kwa karantini hiyo kumeanza juzi majira ya saa 10 jioni baada ya kupokea taarifa kutoka afisa mtendaji wa kata hiyo kwamba zahanati hiyo itafungwa kwa muda ili kumhudumia mtu anayedhaniwa kuwa Ebola.



"Manispaa haikuwa sahihi kuitumia zahanati hii kama karantini ya hofu ya Ebola, hapa kuna shule ya chekechea, sekondari, seminari ya Don Bosco na majirani kama unavyowaona....wasipopewa elimu na kama huu ni ugonjwa wa Ebola watu watakufa sana"alisema.



Sambeke alisema maeneo yatakayoathirika zaidi na kufungwa kwa zahanati hiyo ni Shirimgungani,Cherereni ya Moshi vijijini,Karanga,
Soweto,Bonite madukani na mtaa wa Kigongoni ambapo zahanati huudumia zaidi ya watu 5,000 kwa mwezi.



Kwa upande wake diwani wa kata ya Shirimatunda,Felix Mushi alisema huduma za utoaji wa chanjo ya magonjwa ya Rubella na Surua zimehamishiwa katika ofisi ya mtendaji wa kata hiyo huku wagonjwa wengine wakihamishiwa maeneo mengine.



Alisema tarifa za awali alizopata ni kwamba mtu huyo alipokelewa
katika uwanja wa ndege wa kimataifa Kilimanjaro (KIA), ambapo
alisafirishwa hadi kwenye zahanati hiyo baada ya kudai kuwa na dalili zinazoashiria ugonjwa wa Ebola.



Aidha taarifa zaidi zinadai kuwa wataalam wamechukua sampuli kutoka kwa mgonjwa huyo kwa ajili ya vipimo, ili kujiridhisha, wakati huduma nyingine za matibabu zikiendelea kutolewa kwa mgonjwa huyo anayedaiwa kusafiri kutoka nchini Senegal.



Mmoja wa wakazi anayeishi jirani na zahanati hiyo, Thadei
Sangawe,alisema ameanza kufanya mawasiliano na ndugu wengine waliopo maeneo mengine mkoani humo ili aweze kuhamisha familia yake kuepuka madhara kama ugonjwa huo utakuwa wa Ebola.



"Tunaomba viongozi wenye dhamana hususani madaktari watoe taarifa kwa wananchi juu ya hii hofu iliyopo,maana kukaa kwao kimya kutasababisha wananchi washindwe kuchukua tahadhari na hivyo kusababisha madhara"alisema.



Hata hivyo akizungumza na waandishi wa habari, mkurugenzi wa manispaa ya Moshi Shaban Mtarambe, alisema hayuko tayari kuzungumza kwa maelezo kuwa suala hilo ni la kitaalam zaidi linalohitaji waataala wa kada ya afya kulizungumzia.



Naye mganga mkuu wa manispaa ya Moshi,Dk Christopher Mtamakaya alipohojiwa kuhusiana na taarifa za kuwapo kwa mgonjwa huyo hakuwa tayari kuzungumza zaidi na alipotumiwa ujumbe wa simu ya mkononi alijibu kwa kifupi, huo ni Uvumi.



Kwa upande wake mganga mkuu wa mkoa huo,Dk Mtumwa Mwako alipohojiwa kuhusiana na kuwapo kwa mgonjwa huyo naye alisema hafahamu na aliomba kupewa muda kwani alikuwa katika kikao.



Kuhusiana na suala la mgonjwa huyo,katibu tawala wa mkoa huo, Dk Faisal Isa alisema taarifa za kwanza anapata kutoka kwa mwandishi wetu na akaomba muda wa kufuatilia zaidi.

Lango kuu la kuingia zahanati ya Shirimatunda likiwa na tangazo la kusitishwa kwa huduma za afya katika zahanati hiyo kwa hofu ya kuwapo kwa mgonjwa wa Ebola.
Baadhi ya wagonjwa na wauguzi katika zahanati ya Shirimatunda
wakihamia katika ofisi ya mtendaji wa kata ya Shirimatunda kuendelea na huduma za tiba ikiwamo utoaji wa chanjo ya Surua na Rubella

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Kaka Michuzi asante kwa hii post, please endelea kulifuatilia kwa maana kuna facts za ugonjwa na pia kuna protocol iwapo mtu atakumbwa na ugonjwa huo.
    Awali ya yote tafadhali madaktari watoe elimu haraka sana kuondoa hofu ya ugonjwa huu. Pia familia ya mgonjwa ikiwa ni mgonjwa pamoja na yeyote aliyemhudumia na hasa kama ametapikia mahali, harishia sehemu au kama ametoka damu kama vile wagonjwa wa ebola NA kama mtu alisafisha moja au vyote AU kama mtu alitapikiwa, hariahiwa pasi hilo ndilo la kufuatilia.
    kama ni homa na ni kali sana, siyo rahisi kuambukizwa wakati. Ebola inambukiza kama maji maji ya mwili wa mgonjwa yakigusana na wahudumu ama mtu aliyerukiwa.
    Jamani madaktari toeni semina kwenye radio, internet, misikitini, kanisani, vijijini na sehemu za mihadhara kuelimisha watu ili wajipange sawa!
    Asante Kaka kwa hi nafasi natunaomba wasihi madaktari watusaidi, nilochosema mimi nimetoa kwenye mtandao.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...