Mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Josephine Matiro akiangalia maporomoko ya maji yaliyopo kwenye hifadhi ya Taifa ya Kitulo.
=======
Hifadhi ya Taifa ya Kitulo iliyopo wilayani Makete mkoani Njombe imejipanga vilivyo kuongeza vivutio vipya vya utalii hifadhini humo pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara na njia za kupita watalii ili wafurahie vivutio vilivyopo hifadhini humo. 
Akizungumza mbele ya kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Makete iliyofanya ziara hifadhini humo, Kaimu mkuu wa hifadhi ya Kitulo Bw.Pius Mzimbe (pichani juu) amesema kwa hivi sasa wanazidi kuboresha zaidi hifadhi hiyo ambapo kwa mwaka huu wa fedha 2014/2015 wataboresha barabara zilizopo kwenye hifadhi hiyo ili kusaidia kufikika kirahisi kwa vivutio lukuki vinavyopatikana kwenye hifadhi hiyo hasa kwenye maporomoko ya maji pamoja na kujionea mimea ya aina mbalimbali iliyoota kwenye hifadhi hiyo.
 
 "Kwa mfano kwa sasa tunajenga camp site (vituo vya kupumzikia watalii) ambapo watalii wakiwa hapa watajionea mandhari mabalimbali ikiwemo milima, mimea na vingine, watapanda kwenye milima na kuona maeneo ya mbali na wakichoka watarudi hapa kupumzika na tutawawekea bafu na maliwato kwa ajili yao pamoja na jiko kwa ajili ya kuwapikia vyakula wanavyovipenda hasa vya asili" alisema Mzimbe. 
Amesema kumekuwa na changamoto ya kutofikia baadhi ya vivutio hasa maporomoko ya maji kutokana na ubovu wa barabara wakati wa masika hivyo kwa kuziboresha kutasaidia barabara hizo kupitika muda wote hivyo kuongeza mapato yatokanayo na hifadhi hiyo ya Kitulo. 
 
Bw. Mzimbe ametoa wito kwa wananchi wa ndani na nje ya Makete kujijengea utaratibu wa kutembelea hifadhi hiyo ili wajionee vivutio mbalimbali ikiwemo maua, ndege, maporomoko ya maji na mimea mbalimbali ambayo ipo hifadhini humo tu na vivutio vingine ambavyo wanavigundua siku hadi siku. 
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Makete ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya Mh. Josephine Matiro amesema wilaya yake imebarikiwa kuwa na vivutio mbalimbali vya kitalii ambavyo vipo ndani ya hifadhi ya Kitulo na vingine vipo nje hivyo wao kama serikali watahakikisha vivutio hivyo vinaendelea kuwepo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na cha baadaye. 
 Mh. Matiro amesema ni vyema wanamakete wakajitokeza kwa wingi kufanya utalii wa ndani na kujionea jinsi wilaya yao ilivyobarikiwa na ni jambo la aibu kwa watalii wa nje ya nchi kuja kutembelea hifadhi ya Kitulo ilihali wakazi wa makete hawajawahi kuitembelea. 
 "Kwa mfano leo tumejionea vivutio vingi humu hifadhini, lakini ukipita kwa gari unaishia kuona maua ama ndege lakini ukiingia humu ndani vipo vivutio vingi vya ajabu na vya kuvutia, mimi na kamati ya ulinzi na usalama tumeamua kuonesha mfano, tunaomba wananchi mtuunge mkono kwa kuja kuitembelea hifadhi yetu ya kitulo" alisema Matiro. 
 Wakiwa hifadhini humo wajumbe wametembelea maporomoko ya maji ya Mwakipembo na Numbwe ambayo ni marefu zaidi, pamoja na eneo ambalo linajengwa vituo vya kupumzikia watalii na pia kujione mandhari tulivu ya hifadhi hiyo ya Kitulo. 
 Hifadhi ya Kitulo ipo katika tarafa ya matamba wilayani Makete na inasifika duniani kwa kuwa na maua na ndege na kwa hivi sasa vivutio vingine vya utalii vimekuwa vikiongezeka siku hadi siku. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...